Kocha wa Real Madrid Carlo Ancelotti hakutakiwa kuongelea usajili wa Bale hadharani, kocha wa Tottenham Hotspur Villas-Boas amesema jana Jumamosi.
Ancelotti akizungumza
kwenye mkutano wa waandishi wa habari jijini Los Angeles jumatano
iliyopita alisema wapo kwenye mazungumzo na Spurs baada ya kuibuka kwa
taarifa kwamba wanakaribia kuvunja rekodi ya usajili ili kumsajili winga
huyo huyo wa Wales.
Alipoulizwa kama anahisi Ancelotti hakuwa sahihi, Villas-Boas alisema:
"Nadhani ndio, kwa maoni yangu. Carlo ni mtu ninayemkubali na
kumheshimu sana, lakini hakuwa sahihi kulifanya lile suala la Bale kuwa
hadharani.
"Kuhusu
hizi tetesi kwamba Bale anakaribia kujiunga na Madrid sio kweli kabisa.
Kitu pekee ambacho tumewasiliana na Madrid ni kuwaeleza kwamba mchezaji
wetu hauzwi."
Villas-Boas
alikuwa akizungumza kwenye mkutano wa waandishi wa habari mara baada ya
mchezo wa kirafiki kati ya Tottenham na Monaco ulioisha kwa Spurs
kufungwa 5-2, mchezo ambao Bale hakucheza kutokana na kutokuwa fiti.
"Gareth
ni mtu ambaye nampenda. Tunaongea na Madrid kwa sababu kuna heshima
iliyojengeka baina ya vilabu hivi viwili kufuatiwa uhamisho wa Luka
Modric," aliongeza Villas-Boas.
"Tunajenga
timu nzuri kwa ajili ya msimu ujao. Tunajiandaa kwa Bale kuwa nasi.
Lakini tunajua kwenye soka kila kitu kinawezekana," alisema.
Comments
Post a Comment